Tuesday, June 26, 2012

WATANZANIA

WATANZANIA BADO WANA KIDONDA KINACHOUMA KWA KUUZWA NYUMBA ZA SERIKALI KWA BEI YA KUTUPWA

KAMA ilivyo ada tuanze makala haya kwa kumuomba Mungu atuzidishie siku za kuishi hapa duniani kwani akiamua kutunyang’anya pumzi, tunakwisha wote, hivyo basi inatupasa kumshukuru na kufuata mafundisho yake ambayo yanasisitiza upendo, amani na kumcha yeye.
Baada ya kutamka hayo tuingie katika mada ya leo, Wahenga walisema msema kweli ni mpenzi wa Mungu nami leo nataka niseme kweli kabisa kutoka rohoni.

Nilipata faraja sana wiki mbili zilizopita baada ya kumsikia Mbunge wa Simanjiro, Christopher ole Sendeka akisema  bungeni  Dodoma mwezi uliopita, kwamba anakusudia kuwasilisha hoja binafsi katika kikao kijacho cha Bunge cha Aprili mwaka huu, kulitaka Bunge lipitishe azimio la kurudishwa kwa nyumba za Serikali zilizouzwa katika mazingira ya kutatanisha na serikali ya awamu ya tatu iliyokuwa ikiongozwa na Benjamin William Mkapa.

Mheshimiwa Sendeka ambaye anajipambanua kuwa ni  mmoja wa wabunge ambao wanapambana na vitendo vya ufisadi nchini, akasema hatua hiyo ya serikali kuuza nyumba za watumishi wake haikubaliki siyo tu kwa sababu siyo endelevu, bali pia ina kila dalili za ukiukwaji wa misingi ya uadilifu na utawala bora lakini pia namuongezea kuwa wananchi ambao ndiyo wenye mali hawakushirikishwa.

Ndugu zangu, nasema wazi kuwa kauli ya Mheshimiwa Sendeka  hapana shaka itakuwa imewafariji Watanzania wengi ambao bado wana kidonda na maumivu kwa kuuzwa nyumba hizo za serikali kwa bei ya kutupwa, wananchi hao  walidhani hawana  mtu wa kupigania nyumba hizo za serikali ambazo si mali za fulani bali ni za wananchi wote wa nchi hii.

Nimuambie ole Sendeka kuwa  wananchi wengi wako nyuma yako na wale ambao nawafahamu na nisiowafahamu ambao  walipinga kwa nguvu zote pasipo mafanikio kitendo cha serikali kuuza nyumba hizo, wanakuombea maisha marefu ili azma yako itimie.

Hakuna ambaye hakumbuki kwamba uuzwaji wa nyumba hizo ulipingwa vikali katika kila kona ya nchi yetu siyo tu kwa kuwa ziliuzwa kwa bei ya kutupwa au ya kupasiana kama mpira wa miguu au wa mikono, bali pia zoezi hilo kuna madai kuwa lilifanyika bila kuwa na uwazi na kutofuatwa kwa taratibu zilizowekwa kuhusu uuzwaji wa mali za serikali. Hii ni mbaya sana kwa taifa linalosisitiza amani na mshikamano wa kitaifa.

Wananchi wengi walitafsiri kuwa kwa kuwa walipinga uuzwaji wa nyumba hizo za umma basi wakasema kwamba uuzwaji wa nyumba hizo ulionekana dhahiri kufanywa kibabe. Inawezekana uuzwaji wa nyumba hizo bila shaka ulipata baraka za Baraza la Mawaziri, lakini  kitendo kile tunaweza kutafsiri kwamba kilikuwa ni unyang’anyi na ukwapuaji wa wazi wa mali ya umma kinachoweza kufananishwa na usaliti kwa watu wanaotajwa na katiba kuwa ndiyo wanaoiweka serikali madarakani.

Nasema hivyo kwa sababu viongozi wa serikali ambao ndiyo waliokuwa na dhima ya kulinda mali hiyo ya umma,  waliugeuka umma wa Watanzania, walikaa na kula njama za kujigawia nyumba hizo  ambazo zilijengwa sehemu maalumu katika miji yote nchini ili kuwawezesha viongozi wa serikali kuishi karibu na sehemu zao za kazi kwa lengo la kuleta ufanisi katika utendaji wa kazi zao za kila siku.
Hakika tumuunge mkono Mheshimiwa Sendeka na niseme tu kwamba makala haya hayatoshi kuorodhesha madudu yote yaliyotokana na kitendo hicho ambacho kilichofanywa na viongozi wetu. Ni dhahiri huo ni ufisadi mkubwa.

Hata hivyo, kitendo kile tunaweza kukitafsiri kwa lugha nyepesi kwamba waliofanya vile walitenda kitendo kibaya sana si kwa usalama wa nchi tu bali pia kwa masilahi ya umma na wengine waliochukizwa na uuzajwi ule walisema uuzwaji huo ulifanyika katika staili ya chukua chako mapema na pengine ndiyo sababu nyumba hizo baada ya kuuzwa kwa viongozi wa serikali siku chache baadaye ikagundulika kuwa zinamilikiwa na watu ambao siyo wa serikali kama alivyosema Mheshimiwa Sendeka.

Mheshimiwa Sendeka ambaye ana hoja inayoungwa mkono na  Watanzania wengi sana  ni kwamba uuzwaji huo haukuwa halali, bali ulikuwa ni wizi wa mchana kweupe na waliofanya vile hawakuwa na hata chembe ya huruma kwa taifa na wananchi wake.
 Wananchi wangeweza kulia na wabunge kama wizi huo ungekuwa umeidhinishwa na Bunge ambalo mamlaka yake yanatokana na wananchi wenyewe lakini waliofanya kitendo kile, hata wabunge hawakuwashirikisha kwa sababu walijua kuwa wangegonga mwamba. Hakuna mbunge ambaye angekubali kuidhinisha wizi huo.

Kitendo cha wateule wachache serikalini kukaa na kula njama za kujigawia nyumba za umma, hakika hakielezeki hata kidogo kama ambavyo hakikubaliki kwa namna yoyote ile na ndiyo maana natoa wito kwa wananchi na hasa wabunge wote kuwa hoja hiyo itakapoletwa bungeni iungwe mkono na wabunge wengi bila kujali itikadi ili walionunua wanyang’anywe.

Yapo madai kuwa viongozi walionunua nyumba hizo, kabla ya kununua walikula njama na kuzikarabati kwa kutumia mamilioni ya fedha za serikali kisha kugawiana kama pipi huku wakijua kuna serikali ya awamu nyingine inakuja na itahitaji watumishi wake waishi humo. Matokeo yake mawaziri, majaji na maofisa wengine wakafikia mahotelini ambapo serikali ililipa mamilioni ya shilingi kama siyo mabilioni.

Bila aibu wala woga, hata nyumba zilizokuwa nyeti kama za  mawaziri; makatibu wakuu; wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya; maafisa usalama wa taifa; makamanda wa polisi wa mikoa na wilaya; mahakimu na majaji; na wakuu wengine muhimu ziliuzwa kwa bei ya ‘kutupa’. Nyingi ya nyumba hizo zilikuwa sehemu nyeti kama vile karibu na vituo vya polisi au majengo ya vyombo vya ulinzi na usalama au karibu na boma au wizara.   

Ndugu zangu wote tulishuhudia  viongozi walioteuliwa na serikali ya Awamu ya Nne ya Rais Jakaya Mrisho Kikwete, walijikuta hawana pa kuishi hivyo kulazimika kukodishiwa mahoteli ya kifahari kama vile nchi hii ni tajiri sana hapa duniani.
 Kwa mfano, Waziri wa Mambo ya Ndani, Shamsi Vuai Nahodha aliripotiwa kuishi katika hoteli moja jijini Dar es Salaam na kulipiwa Shilingi milioni 60 kwa mwezi lakini hata wakati serikali ya awamu hii inaanza, mabilioni ya shilingi yalitumika kuweka mawaziri na majaji kwenye mahoteli. Huu ni wizi wa mchana.

Mimi naamini na Watanzania wakiongozwa na wabunge  wenye nia thabiti ya kulinda rasilimali za nchi hii kwa faida ya raia wa sasa na vizazi vijavyo, wataunga mkono hoja binafsi ya Mbunge Sendeka atakapoiwasilisha bungeni.

Wakati Mheshimiwa Sendeka akijiandaa, sisi tulio nyuma yake kwa umoja wetu tuzidi kupiga kelele kupinga uuzwaji wa nyumba hizo hadi zitakaporudishwa serikalini na ikiwezekana wahusika waadhibiwe. Walitumia vibaya sana ofisi za umma, naamini wakijifungia katika vyumba na kutafakari watagundua kuwa walichokifanya ni ubinafsi uliokithiri na kutojali wananchi waliowaweka madarakani.
Jipu limepasuka, siwezi kuwa adui kwa kusema ukweli.

No comments:

Post a Comment